JEZI namba 30, aliyokuwa anavaa
kiungo wa kimataifa wa Rwanda, mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
(DRC), katika klabu ya Simba, Patrick Mutesa Mafisango kuanzi sasa haitakuwa
ikitumika tena kwa heshima ya mchezaji huyo aliyefariki Dunia usiku wa kuamkia
jana, jijini Dar es Salaam.
Hayo yalisemwa jana Mwenyekiti wa
Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage alipokuwa akihutubia mamia ya wadau wa soka
waliohudhuria zoezi la kuuaga mwili wa marehemu Mafisango kwenye viwanja vya
Sigara Chang’ombe, Dar es Salaam, kabla ya kupelekwa Uwanja wa ndege wa
kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, tayari kwa safari ya kwenda kwao, DRC kwa
ajili ya mazishi kesho.
Heshima kama hiyo alipewa kiungo
wa zamani wa kimataifa wa Cameroon, Marc Vivien Foe na klabu yake, Manchester
City ya England alipofariki Dunia Juni mwaka 2003, ambapo jezi namba 23
ilitunzwa moja kwa moja.
Aidha Rage alisema msiba huu ni
mkubwa kwa Simba kwa kuwa mchezaji huyo alikuwa ni muhimili mkubwa kwa timu
hiyo akiwashauri wachezaji na kuwa nao karibu ndani na nje ya uwanja.
“Mafisango alikuwa na mchango
mkubwa kwa Simba na mara ya mwisho klabu kukumbumbwa na msiba mzito namna hii
ilikuwa ni mwaka 1978 ambapo Simba ilimpoteza mchezaji wake mahiri Hussein
Tidwa na ukweli ni kwamba wachezaji hawa tutawaenzi miaka yote na ndio sababu
ya kutotumia tena jezi namba 30 kwa kuvaliwa na mchezaji yoyote,” alisema Rage.
Rage alisema licha ya umahiri wa
Mafisango Dimbani pia alikuwa mchezaji ambaye alitoa mchango mkubwa na hasa
wachezaji wawapo nje ya nchi kutokana na umahiri wake wa kujua lugha mbalimbali
ambapo alikuwa akiwasaidia wachezaji wenzake.
“Ni pengo kubwa kwa kuwa mchezaji
huyo alikuwa akijua lugha nyingi ikiwemo Kiswahili, Kingereza na Kifaransa
na kuwasaidia wachezaji walipokuwa nje ya nchi tutamkubuka sana
Mafisango,” aliongeza.
Kutokana na machungu ya msiba huo
Rage alishindwa kumaliza kusoma risala fupi ya marehemu mara baada ya kuishiwa
nguvu na kumwaga machozi na kupelekea Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo Godfrey
Nyange ‘Kaburu’ kumsaidia kusoma risala hiyo.
“Mfisango ni mchezaji ambaye
alikuwa akijituma nje na ndani ya uwanja na kabla ya kutua Simba Marehemu
aliwahi kucheza soka katika timu mbalimbali ikiwemo Tp Mazembe ya DRC, APR ya
Rwanda , Azam na Simba za Tanzania na pia alikuwa Nahodha wa timu ya Taifa ya
Rwanda ‘Amavubi’ alisema Kaburu.
Wakati wa kutoa heshima za mwisho
katika uwanja wa Sigara maelfu ya watu walijitokeza uwanjani hapo wakiongozwa
na mchungaji Tito Kihame ambaye aliongoza ibada ya kuuga mwili wa marehemu,
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Fenella Mukangara na viongozi
mbalimbali wa serikali na viongozi kutoka klabu mbalimbali za hapa nchini.
Mukangara aliwataka wachezaji wa
Tanzania kujituma na kuwa na moyo kama ambao alikuwa nao Marehemu Mafisango kwa
kujituma na kuwa na jitihada za zaidi nje na ndani ya uwanja kama ambavyo
marehemu alivyokuwa akifanya.
“Kifo chake ni pigo kubwa kwa
Simba na Watanzania kwa ujumla na tunamshukuru kwa kuvuka mipaka na kuona
umuhimu wa kuja na kucheza Tanzania na pia wachezaji wa Simba wasikate tamaa
cha muhimu waendeleze kile ambacho alikiacha marehemu,” alisema Mukangara.
“Ukweli ni kwamba katika familia
ya soka hapa nchini tumepoteza mtu muhimu sana na tunamuombea kwa Mwenyezi
Mungu ampumzishe kwa amani,” alisema Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania
TFF Angetile Osiah.
“Sisi Simba ni watani zetu na
tunakuwa pamoja katika shida na hivyo basi mimi kama kiongozi wa Yanga
nimeiwakilisha klabu nzima na tutaendelea kuwa bega kwa bega na watani zetu
katika kipindi hiki kigumu ila mchezaji Mafisango alikuwa ni mchezaji hodari
uwanjani hivyo basi anastaili kuigwa na wachezaji wengine,” alisema Selestine
Mwesigwa katibu Mkuu wa Yanga.
Nao wachezaji mbalimbali kutoka
timu ya Taifa Taifa Stars walijitokeza na kubeba jeneza la mchezaji mwenzao na
kuliingiza katika viwanja vya Sigara wachezaji hao Juma Kaseja, Jonh Bocco,
Mwinyi Kazimoto, Shabani Nditi, Amiry Maftah, Nurdin Bakari, Agrey Moris na
Juma Nyoso.
No comments:
Post a Comment