LLOYD NCHUNGA BIHARAGU
C/O LLOYD ADVOCATES,
Morogoro/Bibi TIti
Mohamed Rd,7th Floor, J.K. Nyerere Pension towers
P.BOX 75111, Dar-Es-
Salaam,Tanzania.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA
HABARI KUHUSU KUJIUZULU NAFASI YA UENYEKITI WA KLAB YA YANGA.
Ndugu wana Habari, najua kwamba taarifa hii
itawafedhehesha wajumbe na wanayanga wanaotuunga mkono,hasa ukizingatia maamuzi
ya pamoja ya vikao vyetu vya kamati ya utendaji vilivyopita kwamba hakuna wa
kujiuzulu kati yetu mpaka tujue hatma ya mkutano mkuu ambao tulipanga ufanyike
tarehe 15 Julai 2012, ukiachia mbali shinikizo la kujiuzulu linalotolewa na baadhi
ya wazee na wanaojiita vijana wa klab, kwa wajumbe wa kamati ya utendaji, na
hasa mimi kama mwenyekiti.
Nawashukuru wajumbe kwamba tulifanya kazi kwa pamoja
na kwa ushirikiano mzuri, na hata pale tulipotofautiana tulifanya hivyo kwa
hoja na kufikia maazimio ambayo wote tulikuwa tunawajibika nayo.
Tangu tumeingia madarakani tumeweza kushirikiana na
kupata mataji matatu katika kipindi cha mwaka mmoja, yaani; Ngao ya Hisani
2010, Ubingwa wa ligi kuu ya Vodacom 2010/2011, na Ubingwa wa Afrika
Mashariki na Kati (Kagame Cup), 2011. Zaidi ni kwamba tuliuwa uteja kwa watani
wetu wa jadi kila tulipokutana katika ligi ukiachia mbali mechi ya tarehe 6 Mei
2012, ambayo tulifungwa goli 5 bila, na kuleta mtafaruku mkubwa katika klab
yetu.
Hali kadhalika tumeshirikiana mpaka tumeweza
kuboresha mkataba kati yetu na TBL kupitia Kilimanjaro Premium Lager, tumeingia
mkataba na kampuni ya NEDCO kuendeleza mali zetu katika mtaa wa
mafia na uwanja wetu wa KAUNDA baada ya kufikia hatua nzuri katika kupata hati
miliki za maeneo yote mawili. Nafahamu kwamba kampuni hiyo iko katika hatua za
mwisho za kumalizia michoro.
Hali kadhalika tuliingia mkataba wa kuzalisha na kuuza
bidhaa zenye nembo yetu na hasa baada ya kufanya marekebisho yatokanayo na
matakwa ya sheria kule BRELA na pia mkataba na kampuni ya NEXUS LTD, ambayo
itakuwa inatutafutia wadhamini wa nje na ndani, kufanya promosheni zetu na
kampeni kwa njia ya electronic kupitia mitandao mbalimbali na kukusanya data za
wanachama na kusajili wapya tukiwa na malengo ya kukusanya shilingi
300,000,000/= hadi 800,000,000/= kwa mwaka katika kipindi cha miaka mitatu.
Haya yote tuliyafanya tukilenga kujitegemea kujazia mapengo yaliyokuwa
yakitokana na kutegemea ufadhili wa mtu mmoja mmoja.
Kwa ridhaa yenu tumekua tukiendelea na mazungumzo na
makampuni mbali mbali kwa ajili ya udhamini na kwa sababu maalum, nitazitaja
katika hati ya makabidhiano kwa kiongozi ajaye.
Aidha, tumeshirikiana katika kufanya mambo mbali mbali
ya kijamii, ikiwa ni pamoja na sikukuu ya kuadhimisha miaka 77 ya Yanga,
sikukuu za pasaka, kuchangia jamii na waliokumbwa na maafa, na kongamano la
vijana lililolenga kuwaamsha vijana kuitambua nafasi yao katika Yanga ikiwa ni
pamoja na kupata azimio la kuanzisha SACCOSS ya Yanga, ambapo maombi yapo kwa
msajili Manispaa ya Ilala.
Haya yote nayataja ikiwa ni kuwashukuru kwa
ushirikiano na ikiwezekana muweze kuyakamilisha yaliyobaki ambayo mtaona
yalikuwa mazuri.
Lakini pia tulipopata matatizo tulikuwa pamoja.
Nichelee kusema tu kwamba tulisimama pamoja baada ya kujiuzulu Makamu
Mwenyekiti wetu Ndugu Davis Mosha na mjumbe wetu ndugu Seif A. Seif, Ali
Mayayi, na wengineo, kwani tulifungwa na katiba.Tulisimama pamoja pia katika
suala la kujiuzulu ndugu Yusuf M. Manji, aliyekuwa mdhamini mteule na mfadhili
mkuu ambaye sasa ameonyesha nia ya kurudi nanyi mkaridhia mkutane naye. Awali,
tulitumia kila jitihada za kumrejesha lakini ikashindikana.
Hata hivyo doa limetupata baada ya kufungwa na watani
wetu goli 5 bila, ambapo kuna wanachama wanaoelewa na wasioelewa kabisa.
Ninachokiona mimi ni usaliti wa hali ya juu
uliombatana na matukio mbalimbali yaliyopita na yanayoendelea hadi kujaribu
kupindua uongozi wa halali wa kidemokrasia. SIWATUHUMU WACHEZAJI MOJA KWA MOJA,
isipokuwa mfululizo wa matukio wiki tatu kabla ya mchezo ule na sasa,
inaonyesha kwamba kulikuwa na usaliti mkubwa ambao sisi hatukuweza kuubaini
mapema.
Sioni mantiki katika hoja kwamba wachezaji walikuwa
wakidai mishahara, posho n.k. Au ati mtendaji wetu alishikiliwa Arusha
kwa deni la hoteli, ndiyo tuvune bao 5!
Kwa wanaoijua Yanga, imewahi kuwa na madeni makubwa
katika Hoteli mbali mbali, mawakala wa ndege n.k, na baadhi tumeyakuta na sisi
tumekuja tukayalipa. Hii imewahi kutokea kabla na wakati akiwepo mfadhili,
sembuse sisi tulioachwa baki, na bado wachezaji walicheza kwa morali.
Hata hivyo, utamaduni wa kutimuana baada ya matokeo
mabaya ni dhambi ambayo itatula kama hatutaiacha, kwani wenye hila na uchu wa
madaraka wataendelea kutumia mbinu hiyo ili kuuondoa uongozi wa kidemokrasia.
Baada ya mapinduzi kushindikana na TFF kuonya kuhusu
mapinduzi hayo, wazee kupitia msemaji wao , Mzee Akilimali wamesikika katika
kipindi cha Michezo cha Redio moja maarufu hapa nchini wakidai kwamba ni
bora Yanga ishushwe daraja au kufungiwa kuliko mimi kuendelea kuongoza!
Hii imenikumbusha HEKMA ZA MFALME SELEMANI akiamulia
ugomvi wa wanawake wawili waliokuwa wakigombea mtoto naye akaamuru wamgawane
nusu kwa nusu. Yule mwenye mtoto kweli alimuomba Mfalme amuachie mwenzie kuliko
kumkata nusu.
Kwa hekma hiyo nimeamua kujiuzulu nafasi yangu katika
Uenyekiti wa Yanga kwani ni klab ninayoipenda hata kama sio kiongozi kwa
mujibu wa ibara ya 28 ya katiba yetu.
Vile vile siko tayari kuona klab yangu ikisalitiwa au
kuhujumiwa eti kwa sababu tu mimi ni kiongozi.
Natumaini kamati ya utendaji kwa pamoja na wale
tuliowateua chini ya ibara ya 29(3) ya katiba ya Yanga pamoja na bodi ya
wadhamini, itawaongoza wanachama mpaka kufikia mkutano mkuu kwa mafanikio
zaidi.
Nitaendelea kuwa mwanachama mwadilifu na nitatoa
mchango wangu wa hali na mali pale nitakapo hitajika na nikiwa na uwezo
wa kufanya hivyo.
YANGA DAIMA MBELE, NYUMA MWIKO.
Wasalaam,
LLOYD NCHUNGA BIHARAGU.
Nakala kwa:-
Mama Fatma Karume,Mdhamini
Francis Kifukwe, Mdhamini
Bwana Yusuf Manji – Kwa taarifa