Sunday, September 18, 2011

Dhoruba, Chelsea v Man United presha juu!

 
ANDRE Villas-Boas ameanza vizuri Ligi Kuu England, lakini kocha huyo wa Chelsea atatakiwa kujihesabu yeye ni bora kama atawadhibiti Manchester United katika Uwanja wa Old Trafford kesho Jumapili majira ya saa 12:00 jioni.
Manchester United ni timu nzuri zaidi katika Ligi Kuu England msimu huu ikiwa na mshambuliaji machachari Wayne Rooney, ambaye amefunga mabao nane kati ya mabao 18 yaliyofungwa na kikosi hicho baada ya kucheza mechi nne.
Hata hivyo, timu hiyo ambayo ilitoka sare ya bao 1-1 na Benfica katika mechi ya fungua dimba ya Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya makundi, Jumatano wiki hii haitataka kufanya makosa kwa mara nyingine.
Nyota kama Rooney, Javier Hernandez `Chicharito' na Ashley Young watamfanya kocha Villas-Boas akune kichwa juu ya wachezaji gani wanaweza kuwazuia watu hao.
Chelsea tayari imeshinda mechi tatu na kutoka sare mara moja dhidi ya Stoke City, lakini Villas-Boas anajivunia washambuliaji wapya Juan Mata na Raul Meireles, lakini bado anatafuta mtu wa kushirikiana na Fernando Torres ambaye ameshindwa kutamba.
Lakini Villas-Boas anafahamu mtihani unaomkabili, alisema:
Tunakutana na Man United, huenda ni wakati mgumu lakini utakua ni wakati mzuri iwapo tutashinda."
Lakini mara ya mwisho timu hizo zilipokutana Manchester United ilishinda mabao 2-1 katika Uwanja wa Old Trafford na ushindi huo ulichangia kikosi cha Ferguson kupata ubingwa wa 19 wa Ligi Kuu England wiki moja baadaye.
Huku Didier Drogba akiendelea kupona maumivu ya kichwa, kocha Villas-Boas anatakiwa kuwa makini kuwapanga wamaliziaji.
Anaweza kuendelea kumwamini Torres, ambaye alitengeneza mabao mawili katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambayo walishinda mabao 2-0 dhidi ya Bayer Leverkusen lakini akumbuke kuwa nyota huyo amefunga bao moja tu tangu alipojiunga na klabu hiyo Januari mwaka huu.
Lakini, John Terry ambaye alipumzika katikati ya wiki na Frank Lampard, aliyecheza kipindi cha pili kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya wataingia uwanjani.
Beki wa Manchester United, Rio Ferdinand alikosa mechi za karibuni dhidi ya Tottenham na Arsenal kutokana na maumivu ya misuli lakini alicheza dhidi ya Bolton na hakuingia uwanjani dhidi ya Benfica, sasa haijafahamika kama atarudi uwanjani wiki hii.
Kipa David De Gea, hakucheza dhidi ya Benfica, lakini kocha Ferguson amesema atampanga dhidi ya Chelsea na Anders Lindegaard atarudi benchi.
Mabingwa hao watawakosa Nemanja Vidic (kaumia goti) Tom Cleverley (kaumia mguu), Danny Welbeck (kaumia misuli) na Rafael (kaumia bega).
Katika mechi nyingine Manchester City itacheza na Fulham kesho Jumapili, Liverpool itacheza na Tottenham kesho Jumapili. Na Arsenal itacheza na Blackburn Rovers, leo Jumamosi.