Mbunge
wa Jimbo la Ubungo,John Mnyika
. NI KATIKA HUKUMU YA KESI KUPINGA MATOKEO YA
UBUNGE WA JOHN MNYIKA
James Magai
MAHAKAMA Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, leo itawaliza au kuwafurahisha wapenzi na
wanachama wa Chadema wakati itakapotoa hukumu ya kesi ya kupinga matokeo ya
ubunge yaliyompa ushindi Mbunge wa Jimbo la Ubungo kupitia chama hicho, John
Mnyika.
Kesi hiyo namba 107 ya 2010, ilifunguliwa na aliyekuwa mgombea wa CCM, Hawa
Ngh’umbi dhidi ya Mnyika ambaye ni mdaiwa wa pili katika kesi hiyo akitetewa na
Wakili Edson Mbogoro.
Mdaiwa wa kwanza katika kesi hiyo iliyoko mbele ya Jaji Upendo Msuya ni
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na aliyekuwa Msimamizi wa Uchaguzi (RO)
katika jimbo hilo, (aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni) ambao
walikuwa wakitetewa na Wakili Mkuu wa Serikali (PSA), Justice Mulokozi.
Katika uchaguzi huo, uliofanyika Oktoba 31, 2010, Msimamizi wa Uchaguzi,
Raphael Ndunguru alimtangaza Mnyika kuwa mshindi Novemba 2, 2010 baada ya
kupata kura 66,742. Ngh’umbi alipata kura 50,544.
Hata hivyo, Ngh'umbi hakuridhishwa na matokeo hayo akaamua kufungua kesi
Mahakama Kuu kuyapinga, akimtumia Wakili Issa Maige.
Katika hati yake ya madai na wakati akitoa ushahidi mahakamani, Ngh’umbi
na mashahidi wake walidai kuwa kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa taratibu na
kisheria katika ujumlishaji wa kura na utangazaji wa matokeo ambao umeathiri
matokeo hayo.
Hoja za kuzingatia
Katika hukumu ya leo, Jaji Msuya atazingatia hoja tano ambazo zinatokana na
madai katika hati ya Ngh’umbi alizozitoa wakati akitoa ushahidi wake mahakamani
pamoja na mashahidi wake wawili, kuhusu ukiukwaji huo wa sheria.
Hoja hizo zitakazozingatiwa katika hukumu ya Jaji Msuya ni pamoja na kama
mkanganyiko wa takwimu za kura katika Fomu namba 24B (Fomu za matokeo ya jumla
ya ubunge), zimeathiri matokeo hayo ya uchaguzi mzima.
Hoja nyingine ni kama mlalamikiwa wa pili (Mnyika), aliingia na kompyuta
(laptop) tano katika chumba cha majumuisho ya kura na kama ndizo zilizotumiwa
na wasimamizi wa uchaguzi kuhesabu na kujumlishia kura.
Nyingine ni kama marekebisho ya kura katika baadhi ya fomu namba 21B, (Fomu za
matokeo ya kura za ubunge vituoni), yalifanyika katika chumba cha majumuisho na
mlalamikiwa Mnyika kuingia na kundi la wafuasi wake katika chuma cha majumuisho
kinyume cha sheria.
Hoja nyingine ni kama mlalamikiwa wa pili (Mnyika) alitoa kauli za kashfa dhidi
ya mlalamikaji (Ngh’umbi) kwa kumuita fisadi, akimtuhumu kuuza jengo la Umoja
wa Wanawake wa CCM (UWT).
Wakati akitoa ushahidi wake mahakamani, Ngh’umbi alidai kuwa matokeo hayo siyo
sahihi kwa sababu pamoja na mambo mengine, katika fomu ya matokeo
yaliyotangazwa kuna kura 14,854, zisizojulikana mahali zilikotoka ambazo upande
wa mashtaka unadai ni kura hewa.
Alisema kwa mujibu wa fomu hiyo, kura halisi zilikuwa ni 119,823, kura halali
zilikuwa ni 117,639 huku kura zilizokataliwa (zilizoharibika) zikiwa ni 2,184.
Lakini alidai kuwa ukijumlisha kura zake na za Mnyika wote kwa pamoja kisha
zikitolewa kutoka katika kura halali zilizopigwa, zinabaki kura 353 ambazo
ndizo zitagawanywa kwa wagombea wengine 14, jambo ambalo alisema si sahihi.
Hata hivyo, wakati akijitetea, Mnyika alikanusha madai hayo yote licha ya
kukiri kuwepo kwa mkanganyiko wa usahihi na uwiano wa kura katika Fomu namba
24B.
Lakini, bado alidai kuwa dosari hiyo zinaweza kurekebishwa na kwamba haziathiri
matokeo kiasi cha kuyafanya yawe batili.
Shahidi wa kwanza upande wa wadaiwa (DW1), aliyekuwa Msimamizi Msaidizi wa
Uchaguzi, Gaudence Kadiarara alikiri kuwa Mnyika aliingiza kompyuta hizo japo
alidai kuwa hata hivyo, hawakuzitumia, tofauti na Mnyika ambaye alidai
hakuingia na kompyuta yoyote.
Shahidi huyo na mashahidi wengine wa utetezi akiwemo Msimamizi wa Uchaguzi
(Mkurugenzi wa Manispaa), pia walikiri kuwepo kwa mkanganyiko katika fomu ya
matokeo hayo ya ubunge lakini, wakasisitiza kuwa dosari hizo haziathiri matokeo
jumla.
Hoja hizo ndizo ambazo ama zitamshawishi Jaji Msuya katika hukumu yake kutengua
matokeo ya ubunge huo au kuthibitisha kwamba matokeo hayo ni halali.
Mawakili wa utetezi, PSA Mulokozi kwa niaba ya AG na RO na Mbogoro kwa niaba ya
Mnyika, walidai kuwa mlalamikaji ameshindwa kuthibitisha madai yake na hivyo
kuiomba mahakama iyatupilie mbali.
Lakini, Wakili Maige anayemtetea Ngh’umbi alisema wamethibitisha madai yao kwa
kiwango kinachohitajika kisheria na kuiomba Mahakama itengue matokeo hayo
yaliyompa ushindi Mnyika.
Alisema madai mengine yameungwa mkono na mashahidi wa utetezi hususan DW1
aliyekiri Mnyika kuingia na kompyuta katika chumba cha majumuisho ingawa
alikanusha kuzitumia tofauti na Mnyika aliyekana kuingiza kompyuta hizo katika
chuma hicho.
Pia Wakili Maige alihoji sababu ya mawakili wa Serikali kutowaita mahakamani
baadhi ya mashahidi ambao walitajwa na upande wa madai na wa wadaiwa kuhusika
kwa namna moja au nyingine katika mchakato wa uchaguzi huo.
Wakili Maige aliwataja mashahidi hao ambao alidai walikuwa ni muhimu kuitwa
mahakamani kujibu madai na kutoa ufafanuzi wa masuala yaliyowagusa kuwa ni
pamoja na Mkurugenzi wa Uchaguzi na Mtaalamu wa Teknolojia ya Mawasiliano wa
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).
Mkurugenzi huyo alidaiwa kuwa ndiye aliyekagua kompyuta zilizotumika kufanyia
majumuisho ya kura ambazo zilidaiwa kuwa zilitoka Manispaa ya Kinondoni, baada
ya mfumo wa awali ulioandaliwa na Nec kuonekana kuwa haufai.
Lakini, Wakili Maige alidai kuwa kitendo cha kushindwa kumuita mkurugenzi huyo
wa Nec mahakamani kutoa maelezo ya ukaguzi alioufanya na mbinu alizozitumia
kuithibitishia mahakama kuwa katika kompyuta hizo zisingewezekana kuingizwa
taarifa za kughushi ni kinyume cha sheria.
Akirejea kesi ya Stanbic Bank (T) Ltd dhidi ya Woods (T) Ltd namba 48 ya mwaka
2002, alidai kuwa Mahakama ilishatoa mwongozo kuwa ushahidi wa kitaalamu
hauwezi kuthibitishwa kwa maneno matupu mpaka mtaalamu huyo atakapoitwa
kuutolea ufafanuzi.
Wakili Maige alidai kuwa upande wa madai umethibitisha kuwa kompyuta
zisizostahili kisheria ndizo zilizotumika kufanya majumuisho na kwamba ndizo
zilizosababisha kuwepo kwa mkanganyiko uliojitokeza katika fomu ya matokeo wa
kura zaidi 14,000, zisizo na maelezo.