Sunday, September 04, 2011

Samata, Costa kuibeba Stars

 
Mbwana Samata
 
Jackson Odoyo na Ombeni Mgongolwa
MACHO na masikio ya Watanzania leo yatakuwa kwa mshambuliaji Mbwana Samata na beki Victor Costa wakati watakapoiongoza Taifa Stars kusaka ushindi muhimu dhidi ya Algeria kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Samata aliyekuwa na mafanikio makubwa tangu alipotua kwenye kikosi cha mabingwa wa Afrika mara mbili TP Mazembe atarajiwa  kuwa dawa ya ukame wa mabao katika jeshi la Jan Poulsen linalosaka ushindi wa kwa udi na uvumba leo ili kufufua matumaini yao ya kufuzu kushiriki fainali za Mataifa ya Afrika 2012.

Taifa Stars hivi sasa inashika nafasi ya tatu katika kundi D ikiwa na pointi nne sawa na Algeria inayoshika nafasi ya nne ikiwa na pointi nne, timu inayoshika nafasi ya kwanza katika kundi hilo ni Morocco na Jamhuri ya Afrika ya Kati zenye pointi saba wakitofautiana kwa mabao ya kufunga.

Stars imeshinda mechi moja nyumbani dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa mabao 2-1 katika pambano lililopigwa jijini Dar es Salaam, ilitoka sare ya bao 1-1 na Algeria, vile vile Stars ilifungwa bao 1-0 na Morocco kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kocha Poulsen leo atalazimika kumwanzisha Samata aliyefanikiwa kujitengenezea namba ya kudumu kwenye kikosi cha Mazembe na wiki iliyopita alifunga bao kwenye ligi ya Congo na kuisaidia timu yake ya TP Mazembe kushinda 3-1 dhidi ya Don Bosco.

Nyota huyo wa zamani wa Simba, atakuwa akisaidiana na John Boko kwenye kuongoza mashambulizi, lakini pamoja na Poulsen kuhitaji ushindi bado atalazimika kujaza  viungo wengi ili kulinda sehemu ya katikati ya uwanja.

Upande wa ulinzi utakuwa chini ya Costa 'nyumba' aliyerejea nchini na kuonyesha mabadiliko makubwa kwenye ngome ya Simba kwani tangu alipoanza kucheza haijaruhusu bao lolote.

Umakini wa Costa akisaidiwa na Juma Nyoso au Aggrey Morris katikati na pembeni akiwa nahodha Shadrack Nsajigwa, Amir Maftah kushoto utakuwa ukuta imara wa kipa Juma Kaseja.

Nahodha wa Mtibwa Sugar, Shabaan Nditi atakuwa jibu saihihi kwenye kiungo mkabaji kutokana na urefu, uzoefu na umakini wake akisaidiwa na Juma Seif ‘Kijiko’ na Henry Joseph katika kuimarisha shehemu hiyo ya kiungo wa chini.

Tatizo pekee linalomsumbua Joseph kwa sasa ni majukumu tofauti anayopata akiwa Stars na katika klabu yake ya Kongsvinger IF ambako siku hizi anachezeshwa kama beki wa pembeni.